Wadau wa Bima Kanda ya Ziwa watembelea ofisi za kamanda wa polisi mkoa wa Geita

Wadau wa sekta ya bima Kanda ya Ziwa leo Septemba 24, 2025 wametembelea Ofisi za Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita kwa lengo la kuendeleza na kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini (TIRA).
Wadau hao waliongozwa na Bw. Oyuke Phostine, Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Kanda ya Ziwa, ambaye alipongeza uongozi wa Jeshi la Polisi mkoani Geita kwa ushirikiano unaoendelea kuoneshwa katika kutekeleza majukumu ya kusimamia sekta ya bima, hususan katika usimamizi wa bima kwa vyombo vya moto na kudhibiti vitendo vya udanganyifu vinavyoweza kuathiri ukuaji wa sekta bima.
Aidha, Bw. Oyuke alisisitiza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya Jeshi la Polisi na Mamlaka utasaidia kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa bima, pamoja na kuhakikisha sheria na taratibu za sekta ya bima zinatekelezwa ipasavyo.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, SACP Safia Jongo, aliwashukuru wadau wa bima kwa hatua hiyo ya kuunga mkono juhudi za Jeshi la Polisi na kuahidi kuendeleza mashirikiano yenye tija katika kulinda maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Ziara hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa juhudi za Mamlaka ya Usimamizi wa Bima katika kujenga uhusiano wa karibu na taasisi mbalimbali za Serikali ili kuimarisha usimamizi, uadilifu na ukuaji endelevu wa sekta ya bima nchini.