Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
Viongozi Waandamizi wa ARCORP Kutoka Misri Watembelea Sekta ya Bima Tanzania
15 Aug, 2025
Viongozi Waandamizi wa ARCORP Kutoka Misri Watembelea Sekta ya Bima Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), tarehe 14 Agosti 2025 ilipokea ziara ya heshima kutoka kwa viongozi waandamizi wa kampuni ya ARCORP Holdings, kampuni ya kibiashara kutoka Misri inayojihusisha na masuala ya  uwekezaji katika miradi mbalimbali, ikiwemo sekta ya bima.

Ziara hiyo ilifanyika katika Ofisi Ndogo za TIRA jijini Dar es Salaam, ambapo wageni hao walipokelewa na Kamishna wa Bima, Dkt. Baghayo A. Saqware, pamoja na maafisa waandamizi wa TIRA. Kupitia ziara hiyo, ARCORP ilieleza dhamira yake ya kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza miradi ya kisasa itakayosaidia kuongeza ufanisi na kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za bima nchini.

Aidha, ARCORP ilipata nafasi ya kufanya mazungumzo na Umoja wa Kampuni Waandikishaji wa Bima Tanzania (ATI), ambapo walibadilishana mawazo kuhusu fursa za kutumia mifumo ya kiteknolojia ili kuboresha huduma za bima na kuongeza uelewa kwa wananchi.

Kama sehemu ya mashirikiano yake, ARCORP pia inafanya kazi kwa karibu na wadau muhimu wa kitaifa wakiwemo Jeshi la Polisi Tanzania, Idara ya Uhamiaji, na Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA), kwa lengo la kuhakikisha mshikamano mpana katika utekelezaji wa miradi yake nchini.

TIRA inatambua nafasi ya wawekezaji katika kuendeleza sekta ya bima na itaendelea kushirikiana nao ili kuhakikisha masoko ya bima nchini yanabaki salama, imara na yenye manufaa kwa wananchi wote.

TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA