Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
Ushirikiano sekta ya bima na vyombo vya habari wadhihirika
18 Aug, 2025
Ushirikiano sekta ya bima na vyombo vya habari wadhihirika

USHIRIKIANO SEKTA YA BIMA NA VYOMBO VYA HABARI WADHIHIRIKA 
 
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imekutana na Wahariri wa vyombo vya habari leo tarehe 18 Agosti 2025 jijini Dar es Salaam na kueleza mafanikio ya sekta ya bima chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
 
Katika Mkutano huo ulioratibiwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware, aliwasilisha Taarifa ya Maendeleo ya Sekta  ya Bima kwa kipindi cha miaka minne (2021–2024) ambapo alielezea hatua kubwa zilizopatikana katika sekta hiyo ambapo Wahariri Zaidi ya 40 na Waandishi 50 walihudhuria mkutano huo
 
Wakati wa uwasilishaji wa taarifa hiyo Dkt. Saqware amewahimiza wahariri na vyombo vya habari kwa ujumla kuendelea kushirikiana na TIRA akisema kuwa vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee ya kuwa daraja kati ya sekta ya bima na wananchi, na hivyo vina jukumu la kuhakikisha elimu ya bima inawafikia Watanzania wote kwa njia mbalimbali.
 
“Wanahabari mnapaswa kuwa wasemaji wabobezi wa masuala ya bima ili kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi na zenye kuaminika. Kupitia kalamu na majukwaa yenu mbalimbali , wananchi wataweza kuelewa nafasi ya bima katika maisha yao..” Alisisitiza Dkt. Saqware
 
Kupitia mkutano huu na program nyingine zilizoandaliwa na TIRA kwa wanahabari ni wazi kuwa ushirikiano kati ya sekta ya bima na vyombo vya habari utaendelea kuimarika na kuhakikisha mafanikio ya sekta ya bima yanapaziwa sauti na yanafahamika kwa Watanzania wote.
 
Vyombo vya habari vitabaki kuwa sehemu muhimu katika ukuaji wa sekta ya bima nchini, kwani ndio vinavyoiunganisha sekta hii na wananchi. Kwa ushirikiano wa karibu na endelevu, elimu ya bima itaendelea kutolewa ili wananchi washiriki zaidi katika sekta ya bima, na hatimae bima kubaki kuwa nguzo muhimu ya ustawi wa maendeleo ya Taifa.