Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
Tunaanzia chini: TIRA yatoa elimu ya bima kwa kundi la watoto na vijana
18 Apr, 2025
Tunaanzia chini: TIRA yatoa elimu ya bima kwa kundi la watoto na vijana

Watoto na vijana ni kundi moja wapo muhimu la kupewa elimu ya bima kwa sababu ni kizazi cha baadaye ambacho kitakuwa chenye taarifa muhimu na sahihi na hivyo kujua namna bora ya kujikinga dhidi ya majanga yasiyotarajiwa kwa kutumia bima za aina mbalimbali. Kwa kuzingatia hilo leo Aprili 16, 2025. Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania imetoa elimu ya bima kwa wanafunzi waliopo kwenye shirika lisilo la kiserikali linalotoa elimu mbalimbali kwa vijana, watoto na akina mama (CSEE).

Akitoa neno la ukaribisho katika semina hiyo iliyofanyika kwenye ofisi za TIRA Kanda ya Mashariki Meneja wa Kanda hiyo, Bw. Zakaria Muyengi aliwaeleza wanafunzi hao majukumu ya Mamlaka, aina za bima na kuwahimiza kufikisha habari kwa wazazi na walezi wao kuhusu umuhimu wa kuwa na bima mathalani bima ya afya kama kinga wakati wa magonjwa.

Aidha, TIRA iliwapa elimu kuhusu hali ya soko la bima nchini na matumizi ya mifumo  ya huduma za TIRA yani TIRAMIS na ORS, lakini pia walielezwa kuhusu Bima ya Afya kwa Wote na Afisa kutoka NHIF ambaye alieleza kuhusu utekelezaji wake na namna wanavyoshirikiana na TIRA kama msimamizi kuhakikisha wananchi wanapata huduma zinazostahili kulingana na kipato. 

Semina hiyo pia ilikuwa na kipindi cha maswali na majibu ya chemsha bongo iliyopewa jina la “bima challenge” ambapo wanafunzi waliulizwa maswali waliyofundishwa kuhusu bima na waliyojibu ipasavyo walipata fursa ya kujishindia zawadi mbalimbali kama kalenda, diary na pesa taslimu.

Naye Bi. Theresia Assey Katibu wa Shirika la Convetion, Social and Economic Empowerment ameishukuru Mamlaka kwa nafasi ya wanafunzi hao kupata elimu ya bima kwani lengo hasa ni kuhakikisha watoto na vijana wanapata taarifa na elimu sahihi ili waweze kufanikiwa katika nyanja mbalimbali.

TIRA kanda ya Mashariki inatoa huduma mbalimbali za kibima kama kusajili na kutoa leseni kwa watoa huduma za bima na pia kutoa elimu ya bima kwa wananchi wa Dar es Salaam, Pwani na Morogoro ambapo ofisi zao zipo jengo la PSSSF ghorofa ya 3 Barabara ya Sam Nujoma jijini Dar es Salaam.

TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA