Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
TIRA, POLISI Kutumia mifumo ya kuimarisha usalama barabarani
03 Feb, 2025
TIRA, POLISI Kutumia mifumo ya kuimarisha usalama barabarani

Leo, tarehe 3 Januari 2025, Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware, amepokea ziara fupi ya Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Kamanda SACP William F. Mkonda (CO-Traffic-Tanzania), katika Ofisi za Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) zilizopo Mtendeni, Dar es Salaam.  

Lengo kuu la ziara hiyo lilikuwa kujadili na kuweka mikakati ya ushirikiano baina ya TIRA na Jeshi la Polisi Tanzania katika maandalizi ya Kikao Kazi cha Makamanda wa Polisi wa Usalama Barabarani wa Mikoa na Wilaya, ambacho kinatarajiwa kufanyika jijini Dodoma katika wiki ya tatu ya Februari 2025. Kikao hicho kitalenga kuweka mikakati madhubuti ya kupunguza ajali za barabarani na madhara yake kwa watumiaji wa barabara.  

Kamanda Mkonda alisisitiza umuhimu wa elimu ya bima kwa makamanda wa polisi, hasa katika uhakiki wa bima kupitia mifumo rasmi. Aidha, Dkt. Saqware, alipendekeza hatua ya kuunganisha mifumo ya TIRA na Polisi ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa za ajali mara moja pindi zinapotokea. Hatua hii inalenga kuhakikisha waathirika wa ajali wanapata fidia zao kwa haraka, kwani taarifa za ajali zitasomwa moja kwa moja na kampuni za bima kupitia mfumo wa TIRA.  

Mkutano huo utahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Dodoma, akiwemo Mkuu wa Mkoa, Bi. Rose Senyamule, ambaye anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi.  

TIRA Kwa Soko Salama la Bima