Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
Rais Mwinyi apokea Taarifa ya Utendaji wa Soko, aipongeza TIRA kwa kuleta mageuzi kwenye sekta ya Bima
21 Feb, 2025
Rais Mwinyi apokea Taarifa ya Utendaji wa Soko, aipongeza TIRA kwa kuleta mageuzi kwenye sekta ya Bima

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amepokea Taarifa ya Utendaji wa Soko la Bima kwa Mwaka 2023 na kuipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kwa mchango wake mkubwa katika mageuzi ya sekta ya bima. Hafla hiyo ilifanyika katika Hoteli ya Verde, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na wadau wa sekta ya bima.

Katika hotuba yake, Dkt. Mwinyi alisisitiza umuhimu wa sekta ya bima kwenda sambamba na kasi ya serikali zote mbili kwa kutumia ubunifu na teknolojia ili kuongeza ufanisi. Alieleza kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zina dhamira ya dhati ya kuendeleza sekta ya bima kama nyenzo ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi alihimiza kuongeza juhudi katika matumizi ya TEHAMA ili kuboresha huduma za bima na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa. Alisisitiza umuhimu wa kuimarisha utafiti wa vihatarishi ili kubuni bidhaa za bima zinazoendana na mahitaji ya soko, hususan kwa mali za serikali na sekta binafsi.

Dkt. Mwinyi alihimiza TIRA iendelee kupitia sheria na kanuni mbalimbali ili ziendane na mazingira ya sasa na ukuaji wa uchumi wa kidigitali. Alisema kuwa elimu kwa umma kuhusu bima ni nguzo muhimu kwa ukuaji wa sekta hiyo na hivyo ni lazima jitihada zaidi zifanyike ili kuongeza uelewa wa wananchi juu ya umuhimu wa bima.

Akiwasilisha taarifa hiyo Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware, alieleza kuwa TIRA itaendelea kuweka mazingira wezeshi katika soko la bima ili kuchochea ukuaji wa sekta hiyo na kuongeza mchango wake katika pato la taifa. 

Aliongeza kuwa mamlaka imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na wadau wa bima ili kuhakikisha kunakuwa na bidhaa bora zaidi zinazoakisi mahitaji ya wananchi na taasisi mbalimbali.

Dkt. Saqware pia alibainisha kuwa TIRA imefanikiwa kupanua huduma zake kwa kufungua ofisi za kanda Unguja na Pemba, hatua inayolenga kuimarisha usimamizi wa sekta ya bima na kuwahudumia wananchi kwa karibu zaidi. Alisema mamlaka inazingatia mageuzi ya kidigitali kwa lengo la kuhakikisha huduma za bima zinapatikana kwa urahisi na kwa ufanisi zaidi.