"Nawapongeza kwa juhudi zenu, ukuzaji Soko la bima" - Dkt. Saqware katika Mkutano wa mwaka wa Mawakala wa Bima

Dkt. Saqware Afungua Rasmi Mkutano wa Mwaka wa Umoja wa Mawakala wa Bima Tanzania kwa Mwaka 2025
Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware, amefungua rasmi Mkutano wa Sita wa Mwaka wa Umoja wa Mawakala wa Bima Tanzania kwa mwaka 2025, uliofanyika leo tarehe 15 Agosti 2025 jijini Dar es Salaam.
Akifungua mkutano huo, Dkt. Saqware amepongeza jitihada zinazofanywa na wadau wa sekta ya bima akieleza kuwa mawakala wa bima wamechangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa soko la bima, japokuwa bado kunahitajika uwepo wao zaidi hasa katika maeneo ya pembezoni mwa nchi.
Amesema kuwa sekta ya bima ni mhimili muhimu wa ustawi wa kijamii na kiuchumi. Bima hutoa kinga dhidi ya majanga ya kifedha, huchochea uwekezaji, na kutoa ajira kwa maelfu ya Watanzania. Mawakala wa bima, kama daraja kati ya kampuni za bima na wananchi, wanabeba jukumu la kuhakikisha wananchi wanaelewa thamani ya bima, wanapata huduma kwa wakati, na kulindwa dhidi ya hatari mbalimbali.
Kupitia elimu ya bima wanayoipata, Dkt. Saqware amewataka mawakala kuwa mabalozi wa kuhamasisha wananchi kuwekeza kwenye huduma za bima.
TIRA itaendelea kuhakikisha sheria na kanuni zinalinda haki za watumiaji wa huduma za bima, kuhamasisha matumizi ya bima kwa sekta isiyo rasmi, na kutoa mafunzo na vyeti vinavyokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa kwa mawakala.
Aidha, Dkt. Saqware ametoa wito kwa mawakala wa bima kuongeza uadilifu katika kazi, kujifunza kwa kuendelea kutokana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya wateja, na kushirikiana kwa kutumia vyema jukwaa hilo kama chombo cha kubadilishana uzoefu na kujenga misingi imara ya ushirikiano.
Mkutano huu wa mwaka ni fursa ya kutathmini tulikotoka, tulipo, na tunakoelekea kama sekta, na kuwataka washiriki kutumia jukwaa hili kujadili kwa uwazi, kupendekeza maboresho, na kuondoka wakiwa na nguvu mpya ya kuendeleza kazi yao muhimu kwa taifa.