Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
Mkutano Baraza la Wafanyakazi TIRA: Wakumbushwa Uwajibikaji, Ueledi na Uwazi ili kuleta Ufanisi katika sekta
30 Jan, 2025
Mkutano Baraza la Wafanyakazi TIRA: Wakumbushwa Uwajibikaji, Ueledi na Uwazi ili kuleta Ufanisi katika sekta

Wafanyakazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) wameaswa kuendelea kuzingatia ueledi, uwajibikaji, na uwazi ili kuhakikisha sekta ya bima inazidi kuimarika na kuchangia maendeleo ya taifa.

Hayo yameelezwa na Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Baraza la Nne la Wafanyakazi kwa mwaka 2025 unaofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku mbili ukianza leo, tarehe 30 Januari 2025, na unatarajiwa kuhitimishwa kesho, tarehe 31 Januari 2025.

Dkt. Saqware amesisitiza umuhimu wa kutoa huduma bora kwa wateja huku akihimiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kazini. 

“Kipimo cha utoaji wa huduma bora kinaanzia hapa kazini baina yetu wafanyakazi. Hudumianeni vizuri kwani Wafanyakazi wote TIRA tunategemeana ili kuleta ufanisi.”

Mkutano huu umewakutanisha wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi kutoka ofisi mbalimbali za kanda, ukiwa na lengo la kujadili na kupitisha bajeti pamoja na masuala mengine muhimu yanayohusu utendaji wa TIRA.

Pamoja na majadiliano ya bajeti, mkutano huo pia umeleta fursa ya mafunzo mbalimbali kwa wafanyakazi wa TIRA, yenye lengo la kuwanoa, kuwakwamua, kuwajenga uwezo ili kuwahamasisha na kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na tija kubwa katika sekta ya bima na hatimaye kufikia malengo yaliyowekwa.