Kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani; Bima na wanawake, bima na jamii: TIRA yashiriki

Arusha, 2 Machi 2025
Siku ya wanawake duniani itaadhimishwa rasmi kitaifa tarehe 8 machi 2025, jijini Arusha ambapo imetanguliwa na maonesho ya huduma na bidhaa mbalimbali yaliyoanza tarehe 1 – 8 machi 2025, yanayofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini hapo. Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) inashiriki maonesho hayo kama sehemu ya kufikisha elimu ya bima kwa wanawake washiriki na jamii kwa ujumla.
Kwa siku ya pili sasa Mamlaka imeendelea na utoaji wa elimu kwa umma, usikilizwaji wa changamoto mbalimbali za kibima na majibu kwa maswali yahusuyo bima.
Moja, ya mambo muhimu yanayoulizwa ni pamoja na wananchi kutaka kufahamu kuhusu fursa mbalimbali zilizopo katika soko la bima ikiwemo kuwa wakala wa bima ambapo wataalamu wa bima kutoka Mamlaka wanatoa elimu hiyo, vigezo na miongozo mbalimbali inayosimamia na kuwahimiza wananchi kujiunga na fursa hizo.
Washiriki pia wameelezwa umuhimu wa bima katika kulinda mali afya na uwekezaji, ambapo wamesisitizwa umuhimu wa kukata bima za nyumba, vyombo vya moto, bima za afya,bima za kilimo na ufugaji, bima kulinda biashara, bima ya maisha na nyinginezo.
Maonesho pia yamekuwa ya manufaa kwa wadau wenye changamoto za kibima ambapo wamesikilizwa na kupewa utaratibu sahihi mathalani wa kudai fidia ya madai ya bima na madai yao kurekodiwa kwa ufatiliwaji zaidi na Mamlaka.
TIRA inawakaribisha wanawake wafanyabiashara mbalimbali, wafanyakazi na Watu wote kwa jumla kupata elimu ya namna ya kulinda mali zao ili kujikinga na majanga yasiyotarajiwa na kusimama na kauli mbiu ya mwaka huu “Wanawake na wasichana 2025: tuimarishe haki, usawa na uwezeshaji”
TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA