Karibu Katika Uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji wa Soko la Bima 2024 na Jengo la Makao Makuu ya TIRA – BIMA HOUSE

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) inapenda kuwakaribisha wadau wa sekta ya bima, taasisi za serikali, washirika wa maendeleo, na wananchi wote kushiriki katika uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji wa Soko la Bima kwa mwaka 2024 sambamba na uzinduzi wa Jengo jipya la Makao Makuu ya TIRA – BIMA HOUSE, lililopo Njedengwa, Dodoma.
Hafla hii muhimu itafanyika kuanzia tarehe 16 hadi 17 Oktoba 2025, ikihudhuriwa na viongozi wakuu wa serikali, wadau wa sekta ya fedha, na watoa huduma mbalimbali wa bima nchini.
Taarifa hii ni nyenzo muhimu katika kuonyesha hali halisi ya maendeleo ya sekta ya bima nchini, ikiwemo:
- Takwimu za ukuaji wa soko la bima, idadi ya watoa huduma na bidhaa mpya za bima.
- Mwelekeo wa maendeleo ya sekta, changamoto na fursa zilizopo katika kukuza upatikanaji wa huduma za bima kwa wananchi.
- Uwiano wa sekta ya bima na ukuaji wa uchumi wa taifa, ikionesha jinsi bima inavyosaidia kulinda mitaji, ajira, na ustawi wa kijamii.
- Uwazi na uwajibikaji, kwani taarifa hii inatoa picha kamili ya utendaji wa sekta kwa serikali, wadau na umma kwa ujumla.
Taarifa hii inasaidia katika kuboresha Sera na Kanuni zinazohusu sekta ya fedha.
Kwa wananchi, ni fursa ya kujifunza kuhusu nafasi ya bima katika maisha yao ya kila siku, na namna wanavyoweza kunufaika na huduma za bima ili kujilinda dhidi ya majanga ya kifedha.
Uzinduzi wa jengo la TIRA BIMA HOUSE
Uzinduzi wa TIRA BIMA HOUSE ni hatua kubwa kwa TIRA katika kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi na kuimarisha mazingira ya kazi ya kisasa. Jengo hili jipya litakuwa kitovu cha uratibu wa shughuli za usimamizi wa sekta ya bima nchini na kitachangia kuongeza ufanisi, ubunifu na utendaji wa taasisi.
TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA