Kamishna wa Bima akutana na Madalali wa Bima nchini, majadiliano ukuaji sekta ya bima yafanyika

Kamishna wa Bima akutana na Madalai wa Bima nchini, majadiliano ukuaji sekta ya bima yafanyika
Kamishna wa Bima, Dkt. Baghayo Saqware amekutana na Chama cha Madalali wa Bima nchini (Tanzania Insurance Brokers Association) na kufanya mkutano maalum Julai 17, 2025 Onomo Hoteli, jijini Dar es Salaam. Mkutano huo uliandaliwa na chama hicho kujadili masuala mbalimbali katika sekta ya bima nchini.
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na baadhi ya viongozi kutoka TIRA ikiwa ni sehemu ya mfululizo wa matukio ya kujadili mikakati ya kuboresha sekta ya bima nchini, Kamishna wa bima pia akiwa anatekeleza moja ya jukumu la Mamlaka la kulinda haki ya mteja wa Bima.
Viongozi wa TIBA walieleza mambo mbalimbali yakiwemo uboreshwaji wa Miongozo na kanuni mbalimbali za bima nchini ili na wao waweze kuboresha biashara zao. Vilevile wajumbe walibadilishana uzoefu wa kuchochea fursa za ukuaji ndani ya sekta ya bima.
Naye Kamishna wa Bima aliwaahidi wajumbe hao wa TIBA kuwa hatua madhubuti za utekelezaji wa maoni yao zitachukuliwa na kuwaasa kuchukua fursa mbalimbali zinazoletwa na Serikali ya Tanzania chini ya Uongozi wa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi hasa kuhusiana na Usisitizaji wa Bima ya Afya kwa Wote, bima za kilimo na mifugo lakini pia uanzishwaji wa bima za lazima kwenye mikusanyiko ya watu wengi kama vile masoko.
Mwisho Kamishna aliwasisitiza kutumia majukwaa mbalimbali kutoa elimu ya bima kwa wateja, kuongeza upatikanaji wa bima katika maeneo ya vijijini, na ushirikiano na Mamlaka kupitia kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma (PRCU) kwa ajili ya uhamasishaji wa matumizi ya wa bima nchini.
TIRA KWA SOKO SALAMA LA BIMA