Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima Nchini (TIRA), leo imeyafutia leseni ya kufanya biashara za bima makampuni manne na mengine mawili kuwa katika uchunguzi kutokana na kukikuka taratibu na Sheria ya Bima Na.10 ya mwaka 2009.

Makampuni yaliyofutiwa usajili wa kutoa huduma ya ushauri na udalali wa masuala ya bima ni Hans Insurance Brokers, Legend of East Africa Insurance Brokers, Endeavour Insurance Brokers, na Swift Insurance Brokers. Kwa upande wa makampuni ya ushauri na udalali wa bima yaliyochini ya uchunguzi wa Mamlaka kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai ni Pacific Insurance Brokers na Core Insurance Brokers.

Makampuni haya yameshindwa kuwasilisha tozo za bima kwa makampuni ya bima hivyo kuwanyima wateja wa bima haki ya kunufaika na fidia ambazo zingetolewa na makampuni endapo tozo hizi zingewasilishwa.

Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo katika Ofisi za Mamlaka, Kamishna wa Bima Nchini, Dkt. Bhaghayo Saqware amesema kuwa Mamlaka imefikia uamzi huu kufuatia malalamiko mengi yaliyopokelewa na ofisi yake dhidi ya makampuni haya ya ushauri na udalali wa bima.

"Kutokana na malalamiko yanayopokelewa na Mamlaka imeonekana makampuni haya ya ushauri na udalali wa bima yamekuwa yakikiuka taratibu za uendeshaji wa biashara za bima nchini hivyo kuchafua taswira ya biashara hii na kutishia uhai wa soko la bima nchini" alisema Dkt. Saqware.

Mamlaka imetathmini mwenendo wa makampuni haya na kuona ni vema ikachukua hatua za haraka na zilizo ndani ya uwezo wake kwa mujibu wa Sheria ya Bima Na. 10 ya mwaka 2009 kifungu cha 74 ambayo ni kuyafutia leseni makampuni haya.

Pamoja na kuwa tumeyafutia leseni za kufanya biashara ya bima haya makampuni, Mamlaka imewasilisha taarifa za wamiliki wa makampuni haya kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai ili kuhakikisha haki za wateja wa bima na heshima ya soko la bima inalindwa hata kama kampuni hizi zimefutiwa leseni. Hii italinda wateja, wafanyabiashara waadilifu na taifa kwa ujumla, anaongeza Dkt. Saqware.

Kutoka na biashara ya bima nchini kuwa chini ya usimamizi, Mamlaka inatoa wito kwa wananchi kutolalamika na kunung'unika tu pale wanapopatwa na matatizo ya kibima kwa kutokujua wapi pa kwenda kwani Mamlaka kupitia ofisi zake za makao makuu na za kanda iko tayari kusimamia haki za watanzania na wakata bima.

Attachment: