Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepokea msaada wa shilingi mlioni mia moja kumi na tisa (119) kwa ajili ya shule maalum za Unguja na Pemba kutoka kwa sekta ya bima nchini kwa ajili ya ununuzi wa vifaa mbalimbali vitakavyotumika katika shule hizo.

Msaada huo ulipokelewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla kwa niaba ya Rais Mh. Husein Mwinyi katika hafla ya kilele cha Siku ya Bima Zanzibar 2021 iliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni, Jijini Zanzibar.

Alisema kitendo cha maadhimisho ya Siku ya Bima Zanzibar kila mwaka kitasaidia sana katika kuhamasisha jamii kuelewa umuhimu wa huduma za bima sambamba na Mpango Mkakati wa Serekali Kitaifa katika Sekta ya Fedha “The National Financial Sector Master Plan” yenye lengo la kuwafikia asilimia 80% ya watu wenye uelewa wa bima ifikapo mwaka 2025.

Akipokea msaada huo Mhe. Abdulla aliipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) na Sekta ya Bima kwa ujumla kwa kuandaa Siku ya Bima Zanzibar 2021 ambayo imefanikisha uchangishaji wa fedha hizo.

Alichukua nafasi hiyo kuzitaka taasisi nyingine kuiga mfano bora wa sekta ya bima kwa kutenga fedha kwenye bajeti zao kwa ajili ya kutimiza ushiriki wa kijamii ili kuunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwasaidia Wananchi wake hususan wanaoishi katika mazingira magumu.

Wakati huo huo, Makamu wa Pili wa Rais alikabidhi hundi ya shilingi 119m kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na kuutaka uongozi wa wizara hiyo kuhakikisha fedha zilizopatikana zinatumiwa kwa uangalifu na kufuata utaratibu wa matumizi ili kuonesha thamani halisi ya fedha iliotumika kukununua vifaa kwa ajili ya shule husika. 

Aidha, aliaziagiza taasisi za Serikali na binafsi kutumia huduma za bima ipasavyo kupitia makampuni yanayotoa huduma za bima nchini ili kukabiliana na majanga mbalimbali ambayo yanaweza kusababisha hasara.

Nae Naibu Kamishna wa Bima Nchini Bi. Khadija Issa Said alieleza kuwa Sekta ya Bima inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya taasisi za Serikali kutotambua kampuni binafsi za bima jambo ambalo linazorotesha utendaji wa kazi zao za kila siku.

Bi. Khadija akachukua nafasi hiyo kuziomba taasisi hizo kubadili mtazamo kwa kuzitambua kampuni hizo ili kuinua ari kwa kampuni na taasisi binafsi katika kusaidia Serikali kukuza uchumi wa nchi na kufikia maendeleo yaliyokusudiwa.

Alimweleza Mgeni Rasmi kuwa mnamo tarehe 16 Juni, 2021 Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania kwa kushirikiana na sekta ya bima nchini ilifanikisha matembezi ya hisani na kuhitimisha kwa harambee ya kuwachangia watoto wenye uhitaji maalum katika skuli tano za Unguja na Pemba ambapo upande wa Pemba ni  Skuli ya   Pandani  na Michakaweni, kwa Unguja ni Mwanakewerekwe “F” na  Kisiwandui.

Naibu Kamishna wa Bima alisema kiasi cha fedha hizo zilizokabidhiwa kwa Serikali zilikushanywa kupitia mnada maalum kwa lengo la kununua vitu mbali mbali ikiwemo  magari, matengenezo ya madarasa, vifaa kwa ajili ya wasioona na kusikia katika shule tajwa.