Sekta ya bima nchini imechangia shilingi milioni 100 kwa ajili ya Watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao yaani ‘Watoto Njiti’ wakati wa mbio za marathon za bima zilizofanyika hivi karibuni jijini Dar es salaam.
Akitoa salaam za shukrani kwa washiriki wa mbio hizo, Katibu Mkuu wa Wazira ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Prof. Abel Makubi kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhesimiwa Dkt. Dorothy Gwajima alisema Serikali inawapongeza waadaaji wa mbio za marathoni zenye lengo la kuchangisha fedha kwani bado kuna uhitaji mkubwa wa vifaa mbalimbali kwa ajili ya watoto njiti.
Prof. Makubi aliongeza kuwa pamoja na kuwepo kwa mahitaji mengi bado nchi yetu inakabiliwa na tatizo kubwa la vifo vya watoto wachanga chini ya mwezi mmoja ambapo lazima kuwe na jitihada za kupunguza vifo hivi. Alifafanua kuwa vifo hivi vinachangiwa kwa asilimia kubwa sana na watoto wanaozaliwa kabla ya muda, yaani wanaozaliwa kabla ya mimba kufikisha miezi 9.
“Takwimu zinaonyesha kuwa katika ya asilimia 13 -17 ya watoto wote wanaozaliwa Tanzania wanazaliwa njiti” alieleza Prof. Makubi. Aliwaeleza wananchi waliofika katika tukio hilo kuwa watoto hao huitaji huduma maalum za uangalizi wa karibu ili waweze kukua vizuri na kwenda makwao wakiwa na afya iliyoimarika.
Serikali inafanya jitihada mbalimbali katika kuokoa watoto njiti ikiwa ni pamoja na Wizara ya Afya kuratibu progamu mbalimbali ambazo lengo lake ni kupunguza vifo vya watoto wachanga na wale wa chini ya miaka mitano. “Programu hizo ni pamoja na kuanzisha wodi za matibabu za watoto wachanga na watoto waliozaliwa kabla ya muda (neonatal care units and Kangaroo Mother Care ward) kwenye hospitali za wilaya na manispaa, zoezi ambalo linasimamiwa kwa karibu na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto na Wizara ya Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na linaendelea kwenye mikoa kadhaa ya Tanzania, alifafanua Prof. Abel Makubi.
Katibu Mkuu alipongeza jitihada zilizofanywa na wadau katika kukusanya fedha hizi kwa kusema “washiriki wa mbio hizi, mujisikie fahari kwa kuendelea kusaidia watoto wetu na watoto wa wenzetu kuendelea kupata huduma bora. Nawaomba muendelee kuwa na moyo huu wa kuchangia na msichoke kutoa misaada pale msaada unapohitajika”.
Kwa upande wa Kamishna wa Bima Dkt. Mussa Juma alisema Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania ina jukumu kubwa la kuelimisha wananchi wa Tanzania kuhusu huduma za Bima ili waweze kuzitumia katika kulinda biashara, afya, maisha na mali zao. Hivyo fursa kama hii tunaiona ni muhimu sana.
Alimfahamisha mgeni rasmi kuwa mkakati unaofanyiwa kazi na Serikali kwa sasa kupitia Mamlaka ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 watanzania asilimia 50 wawe wanatumia huduma za bima katika nyanja mbalimbali kama zilivyoainishwa katika Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Fedha 2020/2030.
Dkt. Juma alisema kilichotolewa kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ajili ya Watoto njiti ni mchango wa sekta ya bima kuhakikisha kuwa sekta hiyo unarudisha kwa jamii kwa kile wanachokipata na hivyo kuleta tabasamu kwa watoto hao.
Vile vile, Kamishna wa bima alieleza kuwa, shughuli kama hii haifanyiki Tanzania Bara tu, yatafanyika matembezi ya hisani ya Bima huko Zanzibar ili kuleta hamasa na uelewa kwa Wananchi. Katika tukio hili, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti kwa Baraza Mapinduzi Mheshimiwa Dkt Hussein Ally Mwinyi atakuwa Mgeni Rasmi. Pamoja na kutumia njia nyingine na kuwafikia Wananchi mbio za marathoni na matembezi ya hisani ya bima yatakuwa yanafanyika kila mwaka kwenye maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani. Tunaomba Serikali iendelee kutuunga mkono katika juhudi hizi.
Pamoja na kuzitaja changamoto zinazowakabili watotot wachanga Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Muhimbili Prof. Lawrence Museru, aliishukuru sekta ya bima kwa kutoa msaada huo na kueleza kuwa “ni matumaini yangu kwamba kushirikiana kwetu kutaleta mabadiliko chanya katika kutoa huduma kwa watoto wachanga” akiongeza kuwa huduma kama hizi zikiendelea zitapunguza vifo vya watoto wachanga ili tuweze kufikia malengo ya mpango mkakati wa mwaka 2030 wa kuwa na vifo vya watoto wachanga chini ya vifo 12 kwa kila vifo 1000 vya watoto wachanga.
Hundi iliyokabidhiwa na Katibu Mkuu wa Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Prof. Makubi kwa hospitali ya Muhimbili ni michango iliyotolewa na makampuni ya bima nchini kwa kuratibiwa na Umoja wa Makampuni ya Bima(ATI). Wadhamini wengine walioshiriki ni Doris Mollel Foundation na Vodacom.