Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema ili nchi za Kiafrika ziweze kutekeleza vyema mageuzi ya kiuchumi na kukuza ustawi wa wananchi, ni lazima kuwa na sekta na taasisi za Bima zilizo imara na zenye kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya Sayansi na Teknolojia katika karne ya 21.

Dkt. Mwinyi amesema hayo katika ufunguzi wa Mkutano wa Bima kwa nchi za Afrika, uliofanyika katika Hoteli ya Madinat Bahr, ilioko Mbweni mjini Unguja.

Amesema katika kujenga na kuendeleeza uchumi wa kisasa, uwepo wa mfumo, sheria na taratibu madhubuti za uendeshaji wa shughuli za Bima ni muhimu ili kuwapa wawekezaji imani na uhakika wa usalama wa mitaji wanayotaka kuwekeza.

Kwa upande wake Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo Saqware alimhakikishia Mh. Rais kuwa Mamlaka ya bima iko tayari kuendeleza soko la bima kwa kuweka watu wenye ueledi ili kuvutia zaidi wawekezaji katika maeneo ya uchumu wa blue, kilimo na bima mtawanyo. Bima hizo zitanufaisha zaidi wananchi waishio vijijini.

Dkt. Mwinyi alisema pamoja na kuwepo maendeleo katika sekta hiyo, Afrika inapaswa kuendelea kuimarisha sekta hiyo ili iweze kuyafikia makundi yote ya wanachi yanayojishughulisha na shughuli mbali mbali za kiuchumi, hususan katika sehemu za vijijini.