Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewagiza viongozi na wakuu wa Taasisi za serikali kuhakikisha wanakata bima kwa vyombo vyote vya moto vinavyomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mhe. Hemed ametoa maagizo hayo wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya bima Zanzibar amabayo yalianza tarehe 16 Juni 2021 mjini Zanzibar na kutimishwa kwa kutoa misaada mbalimbali iliyowasilishwa na Mamlaka ya Usimamaizi wa Bima - Ofisi ya Zanzibar kwa niaba ya makampuni ya bima na wadau wengie ambapo kiasi cha shilingi Millioni Mia Moja Kumi na Tisa (119,000,000/=) kilikusanywa na kukabidhiwa.

Ameleza kuwa serikali haitosita kumchukulia hatua mtendaji yoyote ikiwa chombo cha serikali kitapata hasara kutokana na uzembe wa maksudi wa kutovikatia Bima.  Alisema        "ninatoa maagizo kwa watendaji wa Serikali, chombo chochote cha Serikali kitakapopata ajali, tukagundua chombo hicho hakina bima, mhusika wa Wizara hiyo atawajibika ipasavyo, malipo yatakayohotajika hayatalipwa na Serikali, yatalipwa kutoka mfukoni mwake binafsi"

Pia, alizitaka taasisi na wasimamizi wa kesi zinazohusu kughushi bima na nyaraka nyingine za Serikali kuchukuwa hatua staiki za kisheria dhidi ya wahalifu hao. "Jeshi la Polisi, Mkurugenzi wa Mashtaka na Mahakama endeleeni kuwa waadilifu katika kusimamia kesi za kughushi nyaraka za Serikali ikiwemo bima zisizofuata na utaratibu".

Alieleza kuwa kuna ukweli kwamba kuna watu wasio waaminifu wanaofanya biashara ya bima bila utaratibu huku wakifahamika na hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi yao. Alimtaka kila mtu kutimiza wajibu wake katika ekeo hilo na kufahamisha kuwa Serikali haitakubali uzembe wala kupoteza fedha kwa namna yoyote ile. Mheshimiwa Hamed aliwaelekeza wahusika kutumia bima vizuri kwa maslahi ya nchi. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitumia fursa hiyo kuzitaka taasisi nyengine kutenga fedha katika bajeti zao kwa ajili ya kutimiza majukumu yao ya ushiriki wa kutoa huduma kwa kijamii ili kuunga mkono Serikali katika kuwasaidia wananchi hususan wanaoishi katika mazingira magumu.