Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
Rais Dkt. Mwinyi apongeza juhudi za TIRA
05 Sep, 2023
Rais Dkt. Mwinyi apongeza juhudi za TIRA

Leo tarehe 4 Septemba, 2023 katika Ikulu ya Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ametambulishwa rasmi Mabalozi wa Bima Tanzania ambapo amepongeza jitihada zinazofanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) katika kukuza soko la bima nchini.
Mhe. Rais Dkt. Mwinyi amesema Mabalozi wa Bima watasaidia kujenga uelewa wa maswala ya Bima kwa Viongozi mbalimbali Serikalini. Aidha Dkt Mwinyi ameipongeza  TIRA kwa kuunda Konsotia Mbili za  Kilimo na Gesi ambapo zitasaidia Kuongezeka kwa upatikanaji wa mtaji katika ulipaji wa fidia na madai ya Bima kwenye sekta ya kilimo  na gesi kwani itawawezesha makampuni ya Tanzania  kuwa na mtaji mkubwa na hivyo kuepuka wananchi kukata Bima za aina hiyo nje ya Nchi kitendo kinachoikosesha Tanzania fedha nyingi. 


“Nawapongeza kwa kupanua wigo na sasa mmeingia kwenye kilimo na gesi kwani Watanzania wengi ni wanajihusisha na kilimo, endeleeni kutoa elimu juu ya konsotia hizi ili kujenga Imani kwa wananchi hatimae pesa nyingi zibakie nchini” A lisema Dkt. Mwinyi.
Awali Akitoa utambulisho wa Mabalozi hao, Dkt, Baghayo Saqware, Kamishna wa Bima Tanzania Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania amewataja kuwa ni Mhandisi Zena Said, Katibu Mkuu Kiongozi SMZ na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Wanu Ameir Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Japhet Hasunga pia Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Dkt. Saqware wakati akielezea taarifa ya Maendeleo ya sekta ya Bima amesema, Mamlaka kwa kushirikiana na wadau wameanzisha Konsotia ya Bima ya Mafuta na Gesi ambapo Vihatarishi vyote vya nishati vinavyotoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama vile vihatarishi kutoka kwa mradi wa LNG vitakatiwa bima kupitia Konsotia ya  bima ya nishati ya mafuta na gesi Tanzania kwa mantiki hiyo  miradi yote ya gesi na mafuta itakuwa na uwezo wa kubakiza Zaidi ya asilimia 45 ya ada zitokanazo na gesi na mafuta.