Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania

TIRA Logo
Uzinduzi wa Konsotia ya Bima ya Kilimo
03 Jul, 2023
Uzinduzi wa Konsotia ya Bima ya Kilimo

tarehe 01.07.2023 katika viwanja vya Nanenane Ipuli Mkoani Tabora KONSOTIA YA BIMA YA KILIMO imezinduliwa rasmi na Mhe. Hussein Bashe (MB) Waziri wa Kilimo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Uzinduzi wa Konsotia ya bima ya kilimo ni sehemu ya mafanikio adhimu ya Wiki ya Kitaifa ya Ushirika Nchini ambapo Konsotia hiyo itaanza kutoa bima za kilimo kwa zao la Tumbaku. Aidha, mazao mengine ya kilimo katika maeneo yote manne yaani mazao, ufugaji, uvuvi, na misitu yatajumuishwa katika Konsotia kwa kadri itakavyoonekana inafaa.

Katika uzinduzi huo wa Konsotia ya Bima ya Kilimo, Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo A. Saqware na Naibu Kamisha Bi. Khadija I. Said wakiambata na baadhi ya viongozi wa Mamlaka, Umoja wa Kampuni za Bima Nchini (ATI) pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya Bima na Kilimo wamehudhuria uzinduzi huo.

Lengo la Konsotia ya Bima ya Kilimo ni kuweka ufanisi katika utekelezaji wa skimu ya Taifa ya Bima ya Kilimo (Tanzania Insurance National Scheme-TAIS) na kuongeza uwezo wa soko la bima la Tanzania katika kutoa bima za kilimo. Aidha, Umoja wa Kampuni za Bima Tanzania (Association of Tanzania Insurers-ATI) wameunda muungano maalum (Konsotia) wa utoaji wa bima za Kilimo ujulikanao kama “Tanzania Agriculture Insurance Consortium-TAIC”.

 Katika hotuba yake Mhe. Bashe Waziri wa Kilimo amesisitiza kuwa ni wakati sasa wa wadau wa Bima kuwa wabunifu na kuja na bidhaa za bima zitakazoweza kuwakinga wakulima juu ya majanga mbalimbali kama vile ukame, na magonjwa ya kilimo. Katika upande mwingine Mhe. Bashe amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Wizara ya Kilimo itatenga fedha kwa ajili ya kuchochea ukataji wa bima za kilimo.

Kwa upande wake Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo Saqware, amesema kuwa Konsotia ya Bima za Kilimo itakuwa ni jukwaa sahihi la kuishauri Serikali kuhusu masuala ya uanzishwaji wa Skimu ya Taifa ya Bima za Kilimo kwa lengo la kuhakikisha mamilioni ya watanzania wanaojihusisha na shughuli za kilimo na wanapata bima stahiki ili kuwakinga na athari za majanga mbalimbali kama vile ukame, mafuriko, na mabadiliko ya tabia nchi.

Pichani ni Mhe. Hussein Bashe Waziri wa Kilimo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo A. Saqware pamoja na wadau wengine wa sekta ya bima na kilimo waliohudhuria uzinduzi huo.

“HONGERENI SANA WADAU WA SEKTA YA BIMA KWA MAFANIKIO MAKUBWA 2023”